Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe Kamishna Msaidizi wa Polisi, Theopista Mallya amemfutia leseni Dereva wa gari lenye namba za usajili T855 DXL Kampuni ya Masihi, inayofanya safari zake Ubaruku -Mbeya – Tunduma na Ileje, Ally Lugenge (56).
Kamanda Mallya amechukua maamuzi hayo wakati akiendelea na operesheni ya ukaguzi wa magari ya abiria kwenye barabara ya Mbeya – Tunduma katika kituo cha ukaguzi wa magari Mahenje kilichopo Wilayani Mbozi.
Gari hilo aina ya Fuso lenye uwezo wa kubeba abiria 45, lilipakia abiria zaidi ya 66 pamoja na mizigo kitu ambacho ni kinyume na taratibu za sheria za usalama barabarani nq pia ni hatari kwa usalama wa abiria.
Hata hivyo, uamuzi wa kumfutia leseni dereva huyo umechukuliwa baada ya kurudia kosa la kuzidisha abiria ambapo awali alipewa onyo kisha kutozwa faini.
Katika tukio hilo, Kamanda Mallya pia aliwakamata makondakta wawili wa mabasi madogo ya abiria Frank Dicksoni (24) na Zakayo Msimwa (21), kwa kosa la kuchanganya abiria na mizigo kwenye gari la abiria.
Aidha, alitoa wito kwa madereva na makondakta kufuata sheria za usalama barabarani bila Shuruti pia aliwataka abiria kujisimamia wenyewe pindi waonapo gari limejaa.
“Wanatakiwa wasipande na sio mpaka wamuone askari ndio watii sheria za usalama barabarani kila mmoja anatakiwa kutimiza wajibu wake ili kupunguza ajali ambazo zinaepukika,” alisema.