Kocha Mkuu wa Arsenal, Mikel Arteta amesema ni aibu kwa VAR kulikubali bao la kwanza la West Ham kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya England usiku wa juzi Alhamisi (Desemba 28) ambapo Washika Bunduki hao wa London walifungwa mabao 2-0.
Tomas Soucek alifunga akiwa ndani ya eneo la Penati akimalizia krosi toka upande wa kushoto ya Jarrod Bowen dakika ya 13 na kuipa uongozi West Ham, lakini haikufahamika wakati wa kutengeneza shambulizi hilo kama mpira ulikuwa umetoka nje ya uwanja.
VAR ilitumia dakika tatu na nusu kufanya marejeo ya tukio hilo kabla ya kulikubali bao hilo, huku Arteta akifichua kuambiwa kwamba taswira za marejeo hazikuwa zinaonekana vizuri hivyo maamuzi ya mwamuzi ndani ya uwanja yanabaki kama yalivyo.
“Sikuona, lakini kitu pekee walichoniambia baada ya kufanya marejeo ni kwamba taswira haikuonekana vizuri,” alisema Arteta kwenye mkutano na waandishi wa habari baada ya mechi hiyo.
“Ni aibu tekilonojia tuliyonayo haioneshi vizuri kwamba kusema mpira ulitoka nje ya uwanja. Imekwisha, hakuna tunachoweza kusema kwa sasa. Tunatakiwa kushinda mechi na hali iliyotokea juzi, imetokea mara nyingi,” alisema.
Arsenal walipiga mashuti 30 yaliyo lenga lango na kugusa mpira mara 77 ndani ya eneo la Penati la West Ham mara nyingi zaidi.