Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, amewataka wazazi nchini kuwajibika kuhusu malezi ya watoto ili kuepusha kuwa na kizazi kisichokuwa na maadili kujenga Taifa imara.

Dkt. Biteko ameyasema hayo hii leo Disemba 31, 2023, wakati akitoa salamu za mwisho wa mwaka kwenye ibada ya jumapili katika Kanisa Katoliki la Parokia ya Bikira Maria Msaada wa Daima Ushirombo wilayani Bukombe Mkoa wa Geita.

Amesema, wakati tukisherehekea Dominika ya familia, wazazi wana jukumu kubwa la kuhakikisha wanatimiza majukumu yao ya kulea familia, na ndio maana hata mafundisho ya dini yameelekeza wajibu wa Baba, Mama, na Mtoto kwenye wajibu wa kila mmoja na kudumisha malezi ya familia na Upendo.

“Niwaombe wazazi tuwalee watoto kwenye maadili na kutimiza wajibu wetu ili kuepusha kuwa na kizazi cha walevi, majambazi kwani Jamii kwa sasa haiko vizuri” Alisisitiza Dkt. Biteko.

Akiwasilisha salamu za mwaka Mpya, Dkt. Biteko amewataka Watanzania na waumini kwa ujumla kumfanya japo mmoja kwenye Jamii kuwa mwenye furaha, kudumisha Upendo, Amani na kusisitiza kumuombea Mhe. Rais Samia na Serikali ili kuendelea kuleta maendeleo kwa wananchi.

Kwa upande wake, Paroko wa kanisa hilo Padri Julius Msobi, alimshukuru Biteko kwa kushiriki ibada hiyo ya misa Takatifu sanjari na jitihada anazozifanya kuhakikisha wananchi wa Bukombe wananufaika na Maendeleo na kumshukuru Rais kwa kuwajali wananchi wa Bukombe.

Polisi Moro wanasa Lori lililosheheni Bangi, Dereva akimbia
Sherehe zisiwasahaulishe mahitaji ya Watoto Shuleni - Maganga