Kocha Mkuu wa ‘Taifa Stars’, Adel Amrouche amemtaja beki wa Young Africans, Abdallah Hamad ‘Bacca’ kuwa ni mchezaji Bora anayecheza eneo hilo Afrika kwa sasa.

Amrouche ameyasema hayo wakati akitangaza kikosi cha Taifa Stars kinachokwenda kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Misri kwa ajili ya kujiandaa na michuano ya Kombe la Mataifa Afrika ‘AFCON 2023’.

Mbali na Bacca, Amrouche amewataja viungo wa Azam FC, Sospeter Bajana na Feisal Salum Fei Toto’ ni wazuri na kudai anamwona mbali zaidi Fei Toto baada ya ‘AFCON 2023’.

Akizungumza saa chache kabla ya kuondoka jijini Dar es salaam kuelekea Misri, Kocha huyo kutoka nchini Algeria amesema anafurahishwa na uwezo mkubwa wa Bacca.

“Ubora wa Bacca alionao sasa na nidhamu yake ya mchezo anazidi kuwa mchezaji mkubwa na mimi namuona mbali. Kwa sasa ukiniambia nikutajie beki Bora Afrika, jina langu la kwanza ni Bacca.”

“Ni mchezaji ambaye ana uwezo wa kutengeneza mashambulizi anakaba na ni mwepesi wa kupanda na kushuka na sio muoga wa kufanya maamuzi,” amesema.

Wakati huohuo, kocha huyo mwenye misimamo mikali alisema Fei Toto, ni mchezaji mkubwa sana hapa Tanzania, ila kilichomkwamisha mwanzo ni changamoto zake za mkataba wakati anatoka Young Africans kwenda Azam FC.

“Nakumbuka nilimuita na kukaa naye kwa ajili ya kumjenga, anatakiwa kusahau yaliyopita awekeze nguvu kwenye mpira kwa sababu ndio ajira yake, namshukuru Mungu amefanya hivyo na ameonyesha uwezo mkubwa.

“Anachokifanya sasa kwenye ligi kama atakiendeleza kwenye michuano ya AFCON 2023, tutakuwa tunazungumzia mambo mengine hapo baadae, sioni kama ataendelea kucheza soka la Afrika ni mchezaji mzuri na bora.” amesema.

Mbali na wachezaji hao wawili pia amemzungumzia Bajana ambaye pia amemtaja ni miongoni mwa wachezaji bora kwenye kikosi cha timu ya taifa na ni hazina.

Man Utd yampa uhuru Varane
Sita waingia mtegoni Real Madrid