Msemaji wa chama cha Ensemble pour la Republique cha Mfanyabiashara maarufu Moise Katumbi, Hervé Diakiese, amesema hakuna ishara yoyote ya mgombea wao kwenda kortini kupinga matokeo ya uchaguzi wa Urais wa DRC.
Diakese amesema wanalazimika kukaa kimywa kwani Mahakama ya Katiba ni chombo cha Rais Felix Tshisekedi ambacho hakitawatendea haki raia wake au wao kama wapinzani kuhusu udanganyifu na kasoro za uchaguzi na kwamba ni sawa na kesi ya Nyani kumpelekea Ngedere.
Amesema, ”mbali na kambi ya Felix Tshisekedi, hakuna mtu makini, hakuna asiyeegemea upande wowote anayeweza kuridhika na kilichofanyika, na kukiita kama uchaguzi wa kuaminika.”
Aidha, inaarifiwa na wachambuzi wa mambo ya kisiasa kwamba changamoto kubwa ya wagombea hao wa Upinzani ni kutoa ushahidi wa kuyapa uzito madai yao, kwamba ni kweli waliibiwa kura.
“Ni vigumu kupata ushahidi kutoka vituo vyote 75.000 vya kupigia kura kwa siku mbili kutokana na ukubwa wa nchi, hali ya DRC inaeleweka wao wanatoaje siku chache za kukusanya ushahidi kama lengo lao si kupindisha haki,” kilihoji chanzo kimoja cha taarifa.