Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko ametoa wito kwa Watanzania kushiriki katika kutoa maoni kuhusu muswada wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa mwaka 2023, Muswada wa Sheria ya Tume ya Uchaguzi wa mwaka 2023 na Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa wa mwaka 2023.

Dkt. Biteko amesema hayo wakati akizungumza na Wananchi wa Wilaya ya Mbogwe Mkoani Geita katika Sherehe za kuaga mwaka 2023 na kuukaribisha mwaka 2024 zilizoandaliwa na Mbunge wa Mbogwe, Nicodemus Maganga ambazo zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali mkoani Geita wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa, Martine Shigella.

“Mhe. Rais amepeleka miswada hii bungeni iliyosomwa wakati wa Mkutano wa Kumi na Tatu wa Bunge na tangazo limeshatoka la kuwaomba wananchi kwenda kutoa maoni yao bungeni kuanzia tarehe 6 hadi 10 Januari 2024 kuhusu marekebisho ya sheria hizi, niwaombe watanzania, nendeni mkatoe maoni yenu ili kujenga Tanzania iliyo bora kuliko kubaki nyuma kulalamika,” asisitiza.

Kuhusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwaka huu, Dkt. Biteko ametoa wito kwa wananchi kuchagua viongozi walio bora na kwamba watu wasigawanyike na kufarakana sababu ya uchaguzi, bali waungane katika uchaguzi huo kwa kuzungumza yale yanayowaunganisha kama vile barabara, maji, umeme na wasiruhusu mtu kupandikiza chuki katikati yao.

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella akiwasilisha salam za Mwaka Mpya 2024 alisema anaridhishwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye wilaya ya Mbogwe ikiwemo miradi ya Elimu, Maji, Umeme, Barabara pamoja na Afya.

Kwa upande wake, Mbunge wa Mbogwe, Nicodemus Maganga, amemshukuru Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati kwa kufika Mbogwe kushiriki na wananchi katika sherehe hizo na kuongeza kuwa wilaya ya Mbogwe imejipanga vizuri katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo Sekta ya Madini kuendelea kufanya vizuri.

Mwakinyo: Rais Mwinyi apewe heshima yake
Maisha: Kanali Doumbouya aamua kuuketisha urais ardhini