Bondia wa ngumi za kulipwa, Hassan Mwakinyo ameiomba Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Zanzibar ‘ZAPBC’ kuweka picha ya Rais, Dk. Hussein Ali Mwinyi, katika mikanda ya Ubingwa wa Taifa, kama heshima ya kurudisha mchezo huo.

Mwakinyo alitoa ombi hilo jijini Dar es Salaam, katika uzinduzi wa pambano lake lilopewa jina la ‘Mtata Mtatuzi’ litakalofanyika Januari 27, mwaka huu dhidi ya Mzimbabwe, Enock Msambudzi.

Mwakinyo na Msambudzi watacheza pambano lisilo la ubingwa la raundi 10, uzito wa kati, litakalopigwa katika Uwanja wa Amaan Complex, Unguja.

Mwanamasumbwi huyo amesema Rais Dk. Mwinyi amekuwa mstari wa mbele katika kuinua michezo, na ana mchango ikiwemo katika ndondi hivyo anapaswa kupewa heshima.

Akizungumzia kuhusu pambano lake, Mwakinyo amesema anaendelea kujifua na atahakikisha anatoa zawadi ya mwaka huu 2024, kwa kuonyesha kiwango bora kwa kumdunda mpinzani wake.

Naibu Katibu wa ‘ZAPBC’, Nasib Amour, amesema ni muda wa mapromota kwenda Zanzibar kufufua na kuendeleza vipaji vya mabondia waliopo huko, sambamba na kuandaa mapambano ya mara kwa mara.

Promota wa pambano, Ramnadhani Bukini, ambaye ni Mkurugenzi wa Shirikia la Utangazaji Zanzibar ‘ZBC’ amesema pamoja na Mwakinyo kuzichapa, kutakuwa na mapambano 11 ya utangulizi likiwemo la wanawake.

Mwakinyo atapanda ulingoni akiwa na kumbukumbu ya kushinda kwa pointi baada ya kumchakaza Kudesa Katembo, katika pambano hilo lilofanyika Aprill 23, mwaka jana.

Mabinti waumwa sikio mbinu kuepuka mimba za utotoni
Wito utoaji wa maoni miswada sheria ya uchaguzi, vyama vya Siasa