Kocha wa Azam FC, Youssouph Dabo, amesema kiwango kilichoonyeshwa na mshambuliajl mpya wa timu hiyo, raia wa Colombia, Franklin Navarro, katika mchezo wa kwanza dhidi ya Chipukizi katika michuano ya Kombe la Mapinduzi, kimemfurahisha.
Nyota huyo aliyesajliwa juma lililopita, akitokea klabu ya Cortulua inayoshiriki Ligi daraja la pill nchini Colombia, aliingia dakika ya 75 akichukua nafasi ya Kipre Junior, na mechi kuisha kwa Azam FC kushinda bao 1-0.
Kwa mujbu wa Dabo, amesema Navarro anahitaji muda wa kuzoeana na wachezaji wenzake kabla ya kufanya makubwa kikosini.
Amesema pamoja na nyota huyo kucheza dakika chache, ameonyesha kiwango kizuri na kuwa tumaini jipya katika kikosi chake, michuano ya Mapinduzi ni muhimu kwake kupata muda mwingi wa kuzoeana na wenzake.
Pamoja na kumwagia sifa Navarro, kocha huyo amesema hajaridhishwa na kiwango cha timu yake katika michuano hiyo, ila anaamini timu itafanya vyema katika siku za usoni.
Katika msimamo wa Kundi A ambalo Azam FC ipo, inaongoza kwa kuwa na alama nne baada ya kucheza michezo miwili kabla ya mechi ya jana Jumanne (Januari 02) ikifuatiwa na Mlandege na Vital’O ya Burundi zenye alama mbili kila mmoja na Chipukizi ikishika mkia kwa kuwa na alama moja.