Beki wa kati wa Simba SC, Fondoh Che Malone amewaambia wachezaji wenzake kutomdharau mpinzani yoyote watakayekutana naye, badala yake kupambana kwa dakika 90 ili kuhakikisha wanapata ushindi.
Kauli hiyo ameitoa baada ya mchezo wa kwanza wa Kombe la Mapinduzi uliopigwa Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar ambao ulimalizika kwa Simba SC kushinda mabao 3-1.
Che Malone amesema kuwa kupitia mchezo huo, kuna vitu vingi vya kujifunza kupitia kwao wachezaji na kikubwa wanatakiwa kumuheshimmu kila mpinzani watakayekutana naye.
Beki huyo kutoka nchini Cameroon amesema kuwa dharau waliyoifanya kipindi cha kwanza kwa kutomuheshimu mpinzani wao JKU ndiyo imesababisha mchezo uongezeke ugumu wa kupata mabao mengi.
Che Malone amesema kuwa wachezaji wenzake wanatakiwa kufahamu, wapinzani nao wanafanya maandalizi ya mechi ili wapate ushindi, hivyo hakitakijirudia tena kitendo hicho.
Mchezo wetu dhidi ya JKU umeongezeka ugumu, kutokana na dharau, kuridhika na matokeo ya awali katika mchezo huo pamoja na mingine ya Ligi Kuu Bara ambayo tumecheza.
Wachezaji wenzangu wanatakiwa kufahamu kuwa wapinzani wetu nao wanajiandaa na hawaji katika kiwanja cha kuchezea mechi kwa ajili ya kufungwa zaidi ya kutafuta ushindi.
Hivyo kama wachezaji tumeliona hilo, kama wachezaji hatutaki kuridhika badala yake tunatakiwa kupambana kwa dakika 90 kwa lengo la kuwapa furaha mashabiki wetu wanaokuja uwanjani kutusapoti.” amesema Che Malone.
Baadae leo Jumatano (Januari 03) Simba SC itacheza mchezo wake wa Pili wa Kundi B dhidi Singidea Fountain Gate, katika Uwanja wa Amaan Complex, kisiwani Unguja-Zanzibar.