Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Ghana, Augustine Okrah ameweka wazi kila kitu ambacho alizungumza na Rais wa Young Africans, Injinia Hersi Said kabla hajamsajili ndani ya klabu hiyo kupitia dirisha hili dogo la usajili.
Okrah ikumbukwe kabla ya kusajiliwa na Young Africans aliwahi kucheza Simba SC kabla ya kuondoka na kurejea tena nchini kwao Ghana na kujiunga na klabu ya Bechem United na sasa ametua Jangwani na kusaini mkataba wa miaka miwili.
Okrah alisema kuwa kabla ya kusajiliwa na Young Africans alikaa na rais wa klabu hiyo kisha wakazungumza kwa marefu na mapana juu ya kuhakikisha kuwa anaifanya Young Africans kuwa tishio na kufanikiwa kusonga mbele kwenye michuano ya kimataifa kuvuka makundi na kufikia hatua ya Robo Fainali.
“Kabla ya kusajiliwa hapa tulikaa kuzungumza na rais ambapo tulizungumza mambo mengi zaidi ambayo yalisababisha niweze kukubali kujiunga na Young Africans, malengo ya timu kwa ujumla ikiwa ni pamoja na mipango ya timu, kitu ambacho kilinishawishi kukubali.
“Mipango ya timu ni kuhakikisha kuwa kimataifa msimu huu inafika katika hatua ya Robo Fainali ni jambo ambalo aliniambia kuwa natakiwa kuwa sehemu ya mchango huo kwa kuwa anaamini uwezo wangu, hivyo kilichobaki ni kwangu kuwaonyesha Wanayanga kazi ambayo imenifanya nije hapa,” amesema Okrah.