Nahodha na Beki wa zamani wa Manchester United, Gary Neville amewataka mastaa wa Liverpool kuhakikisha wanapambana kubaki kwenye mbio za ubingwa wa Premier League pindi Mohamed Salah atakapoondoka.
Mohamed Salah alifunga mara mbili na kutengeneza bao lingine wakati Liverpool ilipoilaza Newcastle 4-2 juzi Jumatatu na sasa anaondoka kwenda kwenye Fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’ akiwa na timu ya Taifa ya Misri. Idadi hiyo imemfanya nyota huyo afikishe mabao 150 katika Ligi ya Premier.
Michuano ya 34 ya AFCON inatarajia kua kutimua vumbi Januari 13 na kumalizika Februari 11, mwaka huu.
The Reds wako kileleni kwa tofauti ya pointi tatu katika msimamo wa Ligi hiyo, baada ya kushinda juzi na sasa wana pengo la pointi tano dhidi ya Man City, ambao wana mchezo mkononi, na Arsenal, hizi ndizo timu pinzani kwenye vita ya ubingwa.
Salah amekuwa na mchango mkubwa katika mbio za Liverpool hadi kileleni mwa msimamo, akiwa amefunga mabao 14 na asisti nane katika michezo 20 aliyocheza msimu huu.
Lakini sasa shinikizo ni kwa washambuliaji wenzake Darwin Nunez, Diogo Jota na Cody Gakpo kuchukua mikoba ya Salah pindi atakapokuwa kwenye majukumu yake ya kitaifa. Watatu hao wana mabao 13 pekee kwenye ligi.
Neville alisema Liverpool wana wachezaji watatu wa viwango vya juu ambao ni Alisson, Virgil van Dijk na Sala.
“Van Dijk amerejea katika kiwango bora katika mwezi huu au miwili iliyopita. Rekodi ya safu ya ulinzi ya Liverpool imekuwa nzuri na wamepiga pasi nyingi safi. Alisson ndiye golikipa bora zaidi duniani.
“Kuna mshtuko kwamba katika theluthi ya sehemu ya mwisho inaweza kuharibika kidogo. Unajiuliza itakuwaje bila Salah?
“Bado wako kileleni mwa ligi na ni lazima wapambane ili waweze kumpa Salah nafasi ya kurejea na kuwa na mafanikio ya kweli kwenye ubingwa,” alisema Neville.