Klabu ya Mtibwa Sugar imesema inatarajia kufanya uboreshaji kwa kuongeza wachezaji saba watakaoongeza nguvu katika kikosi hicho.
Mtibwa Sugar imekuwa kwenye wakati mgumu tangu kuanza kwa msimu huu ikishika mkia kwa pointi nane baada ya kucheza michezo 14 na kati ya hiyo, kushinda miwili, sare mbili na kupoteza 10.
Kwa mujibu wa msemaji wa klabu hiyo, Thobias Kifaru, kutokana na mwenendo mbaya wa timu, benchi la ufundi limeomba uboreshaji wa wachezaji wapya saba wenye uwezo wa kuisaidia timu kuondoka ilipo.
“Tayari benchi la ufundi limekabidhi ripoti yao kwa Kamati ya Utendaji na wameomba wachezaji saba wapya, tayari mchakato wa mazungumzo na nyota kadhaa umeanza na hadi kufika mwishoni mwa juma hili utaanza kusikia habari njema,” amesema.
Kifaru amesema wanaangazia kwenye michuano ya Mapinduzi ambako wameona vipaji vingi na kwenye timu mbalimbali za Ligi Kuu hivyo wanaamini watapata wachezaji wale wanaowahitaji.
Amesema sehemu zilizotajwa na benchi la ufundi zinazohitaji maboreshaji ni Mlinda lango, Mabeki na Mshambuliaji.
Klabu hii imekuwa ikiongoza kwa kuzalisha Vipaji na kuviuza Simba SC na Young Africans lakini kwa upande wao, kila msimu wamekuwa wakipambana kujinasua kutoka kwenye hatari ya kushuka daraja.