Kikosi cha Simba SC leo kinashuka dimbani dhidi ya APR ya Rwanda katika mchezo wa mwisho wa Kundi B wa Kombe la Mapinduzi msimu huu.
Timu hizo zitavaana saa 2:15 usiku katika Uwanja wa Amaan Complex, Unguja visiwani Zanzibar.
Simba SC itaingia katika mchezo huo ikiwa na pointi sita baada ya kucheza mechi mbili, huku APR ikiwa na alama tatu.
Pamoja na Simba SC kuwa tayari imeshakata tiketi ya kucheza Robo Fainali lakini inahitaji angalau sare katika mechi hiyo ili kujihakikishia nafasi ya kuongoza kundi hilo, huku APR ikitaka ushindi au sare ili nayo kujiweka sehemu nzuri.
Katika Kundi hilo, Singida Fountain Gate inaongoza kwa utofauti wa mabao ikiwa pointi sawa na Simba SC, APR inashika nafasi ya tatu kwa alama tatu wakati JKU ikiburuza mkia bila pointi.
Akizungumza mchezo huo, Kocha Msaidizi wa Simba SC, Selemani Matola amesema kikosi chao kinauchukulia mchezo huo kwa umuhimu mkubwa.
Matola amesema anajua mechi hiyo itakuwa ngumu, lakini wanaendelea kukinoa kikosi chao kuhakikisha wanavuna pointi tatu.
“Ni mechi ambayo itakuwa ngumu, APR ni timu ngumu na yenye uzoefu mkubwa na ipo katika daraja moja na sisi, tutapambana kuhakikisha tunapata ushindi,” amesema.
Kocha wa APR, Thierry Froger amesema Simba SC ni timu kubwa na yenye uzoefu, hivyo atakiandaa kikosi chake kucheza kwa akili na mbinu za aina yake.
“Kucheza na kikosi cha Simba SC ni lazima utumie akili sana, utakuwa mchezo mgumu ambao kwangu nitautumia kupima kikosi changu,” amesema.
Katika mechi zilizopita, Simba SC ilianza kwa ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya JKU kabla ya kushinda 2-0 ilipocheza na Singida Fountain Gate wakati APR ikianza kwa kichapo cha mabao 3-1 dhidi ya Singida kabla ya kushinda mabao 3-1 ilipocheza na JKU.