Kiungo aliyewahi kucheza Simba SC ambaye hivi sasa anakipiga Young Africans, Jonas Mkude, ameupongeza uongozi wa timu hiyo kwa kumsajili Augustine Okrah huku akikiri kuwa ni mchezaji mzuri anaweza kuisaidia timu akipewa nafasi ya kutosha.
Mkude anamfahamu Okrah walicheza pamoja Simba SC na amekiri kuwa urafiki wao haukuishia Msimbazi kwani bado alikuwa anamfuatilia hata alipoondoka Tanzania.
“Okrah ni mchezaji mzuri, suala la kupata nafasi ndiyo litakalothibitisha ubora wake ukiangalia alipotoka, ameondoka akiwa kinara wa upachikaji wa mabao, hiyo tu ni ishara nzuri kuwa ni mchezaji wa aina gani.
“Nimefurahi nimekutana naye tena, naamini amekuja kufanya kazi nzuri kama aliyofanya alikotoka sina wasiwasi na uwezo wake siyo mimi tu, hata waliokuwa wanamfuatilia wanaweza kuungana na mimi.” amesema.
Akizungumzia mashindano ya Kombe la Mapinduzi, Mkude amesema ni mazuri na kwa upande wake yamekuwa chachu ya kuonyesha ubora wake kutokana na kukosa nafasi kwa muda mrefu.
“Mashindano ni mazuri hasa timu ikianza kwa ushindi ndiyo morali inazidi kukua tuna kila nafasi ya kufanya vizuri ili kuweza kufikia malengo ya kutwaa taji la mashindano haya msimu huu.” Amesema
Wakati huo huo Okrah hakufanikiwa kumaliza mchezo wake wa kwanza akiwa na Young Africans jana Alhamis (Januari 04), baada ya kuumia akiwa kwenye harakati za kuipambania timu yake dhidi ya KVZ iliyolazimisha matokeo ya suluhu.