Imefahamika kuwa winga Edwin Balua ameaga katika timu yake ya Tanzania Prisons ya mkoani Mbeya na muda wowote atatangazwa Simba SC ambayo imemnunua nyota huyo kwa dau la Shilingi Milioni 50.

Kiungo huyo anatarajiwa kuwa mchezaji wa pili kutangazwa kuichezea Simba SC, katika dirisha hili dogo lililofunguliwa Desemba 15, mwaka jana baada ya kiungo mshambuliaji wa JKU, Salehe Karabaka kutambulishwa hivi karibuni.

Pia Simba SC wako mbioni kumtambulisha Ladack Chisamba kutoka Mtibwa Sugar.

Nyota huyo huenda akajiunga na kambi ya timu hiyo muda wowote kutoka sasa huko Unguja, Zanzibar ambako wanacheza Kombe la Mapinduzi baada ya taratibu zote kukamilika za usajili.

Taarifa zinaeleza kuwa, winga huyo amesaini miaka miwili kwa dau hilo la Shilingi Milioni 50 baada ya kufikia makubaliano ya pande zote mbili mchezaji na timu yake ya Prisons iliyokuwa inammiliki.

Mtoa taarifa huyo amesema kuwa, usajili huo ni kwa mujibu wa Kocha Mkuu wa timu hiyo, Abdelhak Benchika ambaye alipendekeza winga mzawa.

Ameongeza kuwa bado uongozi wa timu hiyo, unaendelea na usajili huku nguvu nyingi wakielekeza kwa mshambuliaji na kiungo mkabaji wote wa kigeni maalum kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

“Kilichobakia kwa Balua ni kutambulishwa pekee, lakini taratibu zote za usajili zimekamilika kwa asilimia kubwa, ni baada ya viongozi wetu wa Simba SC kukamilisha taratibu zote.

“Ofa nzuri ya Shilingi Milioni 50 ndiyo imemshawishi asaini mkataba huo wa miaka miwili, baada ya Prisons kubariki kusaini mkataba huo Simba SC.

“Balua amesajiliwa kwa mujibu wa mapendekezo ya kocha na siyo viongozi ambao kazi yao ni kutimiza majukumu yao katika kumpatia fedha ya usajili pekee,” amesema mtoa taarifa huyo.

Ahmed Ally ambaye ni Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC, amesema kuwa: “Kila usajili unaokamilika tunauweka wazi, hivyo usajili wa Balua ukikamilika basi tutaweka wazi, kikubwa tunataka kukijenga kikosi chetu ili kiwe imara katika dirisha hili dogo.”

Balua akiwa anaichezea Prisons, amecheza michezo 26 amefunga mabao saba na ametoa asisti sita, kwa maana hiyo amehusika kwenye mabao 13.

Habib Kyombo: Kazi ndio imeanza Kombe la Mapinduzi
RC Sendiga, Wananchi wakubaliana jambo Gendabi