Kikosi cha Kagera Sugar kesho Jumamosi (Januari 06) kitarajea kambini, huku benchi la ufundi la timu hiyo likisema halitasita kuchukua hatua za kinidhamu kwa wachezaji watakaochelewa kuripoti.
Timu hiyo iliyomtema aliyekuwa Kocha Mecky Maxime kutokana na matokeo yasiyoridhisha kwa sasa inashika nafasi ya 14 ikiwa na pointi 13 baada ya michezo 13, iliwapa mapumziko wachezaji baada ya mchezo dhidi ya Young Africans kuahirishwa.
Kocha msaidizi wa timu hiyo, Marwa Chamberi amesema kila mchezaji alipewa utaratibu wa kuwahi kambini, hivyo zipo hatua zitakazochukuliwa kwa yeyote atakayekiuka masharti ikiwamo adhabu ya kukatwa mishahara.
Amesema wameamua kuwahi mazoezini kutokana na hali waliyonayo ya matokeo yao kutoridhisha hivyo itawapa wakati mzuri kusahihisha makosa kabla ya kuanza kwa ligi na mashindano mengine.
“Adhabu zipo ikiwamo kukatwa mshahara, lakini hii ni kazi lazima kila mmoja awahi kutimiza wajibu wake, hatujawa na matokeo mazuri, hivyo lazima tuwahi kujiandaa na ratiba tuliyonayo,” amesema Marwa.