Mabadiliko ya Benchi la Ufundi yametajwa kuwa sababu iliyochangia kwa kiasi kikubwa kikosi cha Namungo FC kutofanya vizuri, huku ikielezwa ujio wa kocha mpya, Mwinyi Zahera utasaidia kufikia nalengo ya kumaliza Ligi Kuu Bara nafasi tano za juu.
Namungo FC ilianza maandalizi ya msimu chini ya Denis Kitambi ambapo wakati ligi inaanza uongozi ulimpa kibarua Cedrick Kaze ambaye baadaye alitangaza kung’atuka kutokana na matokeo mabovu.
Hata hivyo, baada ya Kaze kutimka, kijiti kilikabidhiwa kwa Kitambi ambaye naye alifikia hatma ya kukabidhi mikoba na kujiunga na Geita Gold huku nafasi ikizibwa na Zahera anayetokea Coastal Union.
Nahodha wa timu biyo, Jacob Massawe amesema licha ya wachezaji kupambana na kulinda heshima ya klabu, lakini hawajafikia lengo lao ya kuwa nafasi tano za juu hadi sasa.
Amesema mabadiliko ya mara kwa mara kwenye benchi la ufundi ndio yaliwapa wakati mgumu wachezail kuweza kuelewa falsafa za makocha na kujikuta katika mechi 14 wakivuna pointi 12.
Tulianza na Kitambi, wiki moja hivi kabla ya ligi akaja Kaze, sasa wachezaji tulishindwa kuendana na mabadiliko hayo ndio maana malengo yetu hayakutimia ipasavyo, alisema staa huyo wa zamani wa Stand United.