Nyota wa zamani wa Algeria, Rabah Madjer ametoa maoni yake kuhusu fainali za mataifa ya Afrika (Afcon) zinazotarajia kuanza Ivory Coast Januari 13 kuwa zitakuwa ngumu.
Mashindano hayo yanayotazamiwa kumalizika Februari 11 yatajumuisha timu imara za soka katika Afrika na yatakuwa na ushindani mkali.
Akizungumza na CAFOnline.com, Madjer, mshindi wa tuzo ya mwanasoka bora wa mwaka wa Afrika mwaka 1987, ametabiri michuano hiyo itakuwa migumu kwa sababu mataifa yote makubwa katika soka Afrika yatashiriki.
Madjer amesema ugumu wa michuano hiyo unatokana na ukweli ya kwamba mataifa yote imara katika soka la Afrika yatashirki wakiwemo wenyeji Ivory Coast.
“Nina imani na ubora wa mashindano ya mwaka huu kwa sababu timu zote imara katika soka la Afrika zitashiriki. Mataifa yote shiriki yatagombania ubingwa na natazamia timu zitaongeza viwango kuhakikisha yanakuwa na msisimko,” amesema Madjer.
Amesema kutabiri timu itakayochukua ubingwa ni ngumu hasa ukichukulia uwepo wa timu nyingi bora kwenye mashindano hayo na kuzipa nafasi kubwa timu za Ivory Coast, Algeria, Morocco, Senegal na Nigeria.