Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Ghana Augustine Okrah anaendelea vyema na huenda akatumika katika mchezo unaofuta wa Kombe la Mapinduzi, ambapo Young Africans itakutana na APR ya Rwanda kesho Jumapili (Januari 07).
Okrah aliyesajiliwa Young Africans katika kipindi hiki cha Dirisha Dogo, alipata majeraha katika mchezo dhidi ya KVZ ambapo aligongwa kiwiko kwenye maeneo ya kichwa, jambo ambalo lilimfanya kushindwa kuendelea na mchezo huo.
Akizungumza kisiwani Unguja-Zanzibar Ofisa Habari wa Young Africans, Ally Kamwe amesema kuwa: “Mchezaji wetu Okrah kwa sasa anaendelea vizuri baada ya kupata majeraha ambayo hayakuwa makubwa sana, kwa kuwa aligongwa kwa bahati mbaya kwenye kichwa na akawa damu puani.
“Hivyo hali hiyo ilimfanya asiendelee kucheza lakini nimeongea na daktari wa timu ameniambia kuwa matatizo aliyoyapata Okrah sio makubwa sana, hivyo atauwahi mchezo utakaofuata ambao Young Africans tutacheza kesho Jumapili (Janauri 07) dhidi ya APR.
“Okrah mwenyewe anatamani kucheza mchezo unaofuata na yeye mwenyewe ameniambia hata kama anaumwa lakini ikitokea kuwa watakutana na Simba SC katika hatua ya Robo Fainali, basi yupo tayari kucheza mchezo huo hata kama atakuwa na plasta kwenye pua zake, hii inaonyesha kuwa anatamani kuisiadia timu,” amesema Kamwe.