Uongozi wa Tabora United umechimba mkwara kuwa katika kipindi hiki cha usajili watafanya usajili tishio, ambao utaongeza makali kwenye kikosi chao.
Uongozi huo umeongeza kuwa kikosi chao kwa sasa kipo kwenye mapumziko ya siku 10 kupisha michuano ya Mapinduzi inayoendelea visiwani Zanzibar, huku wakitarajia kurejea kambini kesho Jumapili (Januari 07).
Ofisa Habari wa Tabora United, Pendo Lema amesema kuwa: “Katika kipindi hiki cha mapumziko tumewapa wacheaji wetu mapumziko ya siku 10, kama tunavyojua mikiki mikiki katika ligi yetu ni migumu sana, kwa hiyo baada ya siku hizo kumi kuisha wachezaji watarejea na kuendelea na mazoezi, Kesho Jumapili (Januari 07) watarudi kambini na Jumatatu (Januari 8), tutaanza mazoezi.
“Dirisha la usajili lipo wazi tangu Disemba 15, kwa hiyo licha ya kuanza kwa mazoezi pia tutafanya usajili tishio kwa klabu nyingine, lengo letu ni kumaliza tukiwa katika nafasi nne za juu na ikishindikana kabisa basi tusalie katika ligi tuendelee kutoa burudani kwa Wanatabora.”