Beki wa kati wa Simba SC, Che Malone amevunja ukimya na kueleza kuwa hana ugomvi na kipa wa timu hiyo, Ally Salim na kilichotokea katika mchezo wa Kombe la Mapinduzi dhidi ya Singida Fountain Gate ni kutimiza majukumnu yao.
Katika mchezo huo Simba SC ilishinda mabao 2-0 na kujihakikishia nafasi ya kucheza Robo Fainali ya michuano hiyo inayoendelea visiwani Zanzibar.
Katika dakika ya 65 ya mchezo huo, Che Malone alikaribia kuwazawadia bao wapinzani wao Singida Fountain Gate baada ya kuzembea kuuondosha mpira eneo la hatari hadi kipa huyo alipouwahi mpira na kuudaka. Baada ya tukio hilo, Salim alionekana kumfokea beki huyo.
Akizungumza kisiwani Unguja-Zanzibar, mchezaji huyo amesema kilichotokea ni kukumbushana na kuongeza umakini sababu ulikuwa mchezo mgumu kutokana na malengo waliyokuwa nayo ya kutinga Robo Fainali ya michuano hiyo.
“Hatuna ugomvi na Ally, vile ni vitu vya kawaida kutokea ndani ya uwanja na tulikuwa tunakumbushana, unajua presha ilikuwa kubwa na timu tuliyokuwa tunacheza nayo ilikuwa inahitaji kuweka heshima dhidi yetu,” amesema Che Malone.
Beki huyo aliyejiunga na Simba SC mwanzoni mwa msimu huu akitokea Coton Sport ya kwao Cameroon, amesema haoni sababu ya kulikuza jambo hilo kwani baada ya mchezo walizungumza na kulimaliza wakiwa palepale uwanjani.
Simba SC jana Ijumaa (Januari 05) ilikamilisha mechi za hatua ya makundi, kwa kucheza na APR ya Rwanda na kuambulia sare ya bila kufungana, huku hadi sasa ikiruhusu bao moja katika mechi tatu ilizocheza kwenye michuano hiyo ambayo kilele chake ni Januari 13 Uwanja wa Amaan Complex.