Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini – LATRA, imeyasimamisha magari yote ya Kampuni ya Kilimanjaro Express kutoa huduma ya usafirishaji kutokana na kukiuka masharti ya leseni ikiwamo kutotoa tiketi ya kielektroniki na kuzidisha nauli kwa abiria.
Agizo hilo limetolewa leo na Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, Habibu Suluo baada ya kufanya ukaguzi wa kushtukiza katika stendi ya mabasi ya Magufuli pamoja na ofisi za mabasi ya Kampuni hiyo iliyopo Shekilango jijini Dar es Salaam.
Amesema, mabasi hayo pekee ndio bado yanatoa tiketi zisizo za kielektroniki na kwamba yamebainika kukiuka masharti mengi ya leseni licha ya kuonywa mara kwa mara na kutozwa faini.
“Na leo tumelikamata gari jingine la kampuni hii ya Kilimanjaro inayofanya safari zake Dar es Salaam kwenda Moshi na Arusha likiwa limezidisha nauli kwa abiria, kila abiria alilipishwa nauli tofauti, tukawataka wawarejeshee nauli zao, wakakubali, lakini muda mfupi tumetoka kwenye ofisi zao wakakataa tena kurejesha eti mpaka bosi wao aseme.”
Suluo ameongeza kuwa, “hii siyo mara moja, wamekuwa wakifanya hivi mara nyingi na tumewaonya mara kwa mara na anaona kulipa faini ni kawaida kwake. Sasa sisi lengo letu ni kutaka wafuate sheria na masharti ya leseni, watoe huduma bora na siyo kutoa faini.”
“Na kama anaona kulipa faini ni kawaida kwake sisi hatuwezi kuvumilia, tumetoa maagizo asitoe huduma kuanzia jumatatu mpaka atakapofanya maboresho na kufuata masharti ya leseni yake,” aliongeza Suluo.