Simba SC inatarajia kushuka dimbani leo Jumatatu (Januari 08) kuikabili Jamhuri FC katika mchezo wa Robo Fainali ya Kombe la Mapinduzi utakaochezwa New Amaan Sports Complex, Zanzibar majira ya saa mbili na robo usiku.
Aidha, bingwa mtetezi wa Kombe la Mapinduzi, Mlandege ilikuwa timu ya kwanza kutinga Nusu Fainali baada ya kushinda kwa Penati 3-2 dhidi ya Kikosi cha Valantia Zanzibar (KVZ) katika uwanja huo jana Jumapili (Januari 07), huku APR ikifuatia baada ya kuifunga Young Africans 3-1.
Simba walifuzu Robo Fainali wakiwa kinara wa Kundi B kwa pointi saba baada ya, kushinda michezo miwili na kupata sare moja.
Wanakutana na Jamhuri FC, ambayo imeingia kama mshindwa bora ikiwa imeshinda mchezo moja pekee na kufungwa miwili katika Kundi B.
Kocha Msaidizi wa Simba SC, Seleman Matola amesema ni mechi ngumu unapofikia hatua ya mtoano hivyo wamejiandaa vema ili wasiondolewe.
Kuhusu Babacar Sarr na Aubin Kramno amesema hawatakuwa sehemu ya mchezo wa leo Jumatatu (Januari 08), kwa sababu bado hawajafanyiwa vipimo na madaktari ili kujua afya zao. Na pia kujua afya ya Kramo kama majeraha yake yamepona kabisa.
Kuhusu tatizo la umaliziaji wa nafasi wanazotengeneza, Matola amesema wanaendelea kulifanyia kazi mazoezini na anaamini kwenye mchezo wa leo Jumatatu (Januari 08) mabao yatapatikana.
Mchezo mwingine wa Robo Fainali utakaopigwa leo utakuw akati ya Azam FC dhidi ya Singida Fountain Gate, majira ya saa kumi na robo jioni.