Shirikisho la Soka nchini Tanzania ‘TFF’, limesema utulivu na ubora wa timu ya taifa ya Misri ndio uliofanya kwenda kuweka kambi nchini humo.

Taifa Stars imeweka kambi Cairo kwa ajili ya kujiandaa na fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’ zitakazofanyika nchini Ivory Coast kuanzia Januari 13 hadi Februari 11 na jana Jumapili (Januari 07) walicheza mchezo wa kujipima dhidi ya Misri na kukubali kupoteza kwa 2-0.

Akizungumzia kambi hiyo Katibu Mkuu wa TFF, Kidao Wilfred amesema sababu ya kuweka kambi Misri ni kutafuta utulivu kwa wachezaji, lakini vilevile ni urahisi wa kupata mechi za kujipima nguvu.

“Kwenye mashindano tunaanza na Morocco na ukiangalia wachezaji wa Kaskazini mwa Afrika wanafanana, hivyo Misri ni kiwango sahihi kujipima nao kwa sababu ni miongoni mwa timu kubwa na zenye wachezaji wazoefu,” amesema Kidao.

Naye Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Hamis Mwinjuma ‘Mwana FA’ ambaye yupo Misri amesema Taifa Stars imejiandaa kuliko wakati mwingine ambao imewahi kushiriki mashindano hayo.

“Timu yetu nafikiri imejiandaa kuliko wakati mwingine wowote ambao imewahi kushiriki kwenye Fainali za Mataifa ya Afrika”, amesema.

Tanzania kwa sasa inakamilisha maandalizi yake katika mji mkuu wa Misri, Cairo baada ya kufuzu kwa mara ya tatu, mara ya kwanza nchini Nigeria mwaka 1980 na ile ya mwaka 2019 nchini Misri, ambayo yote waliishia hatua ya makundi.

Taifa Stars ambayo inashiriki mashindano ya 34, mchezo wa kwanza watacheza Januari 17 dhidi ya Morocco, mchezo wa pili Januari 21 dhidi ya Zambia na mchezo wa tatu Januari 24 dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia Congo (DRC).

Dabo: Hautakuwa mchezo wa kisasi
Simba SC kuisaka Nusu Fainali Zanzibar