Kocha wa Nigeria Mreno, Jose Peseiro amesema kuwa timu yake imedhamiria kushinda taji la Kombe la Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’ ili kupunguza pengo la washindi mara saba Misri na washindi mara tano Cameroon.

Timu ya taifa ya Nigeria, Super Eagles, ambao ni mabingwa mara tatu wa AFCON, itakabiliana na kibarua katika Kundi A pamoja na wenyeji Ivory Coast, Guinea ya Ikweta na Guinea-Bissau.

Tutapambana kushinda Kombe la Mataifa ya Afrika ingawa tunatarajia haitakuwa jambo jepesi, “amesema Peseiro alipozungumza na Cafonline.

“Kundi letu ni gumu kwa sababu tunacheza dhidi ya wenyeji Ivory Coast ambao wana kikosi chenye wachezaji wenye vipaji, “amesema.

Hadi sasa Nigeria inashiriki mashindano hayo kwa mara ya 20, ikitwaa taji mara tatu mwaka 1980, 1994, na 2013.

Super Eagles itaanza kampeni zake za AFCON 2023 kwa kucheza dhidi ya Guinea ya Ikweta Januari 14, ikifuatiwa na mchezo dhidi ya Ivory Coast Januari 18 na dhidi ya Guinea-Bissau Januari 22.

Peseiro amekiri kuwa Guinea ya Ikweta, ambayo ilifika Robo Fainali katika AFCON iliyopita, imekuwa na matokeo bora hivi karibuni kuliko hata Nigeria.

Kocha Azam FC apongeza usajili wa Sarr
Andre Ayew avizia rekodi AFCON 2023