Kocha Mkuu wa Azam FC, Youssoupha Dabo, ameupongeza Uongozi wa Simba SC kwa kufanikisha usajili wa jembe ‘jipya’ lililosajiliwa klabuni hapo, Babacar Sarr na kuweka wazi huo ni usajili bora uliofanywa na Wekundu hao wa ‘Msimbazi’ katika kipindi hiki cha Dirisha Dogo.

Uongozi wa Simba juzi Jumamosi (Januari 06) walimtambulisha rasmi kiungo huyo raia wa Senegal na jana Jumapili (Januari 07) kumpeleka visiwani Zanzibar kujiunga na wachezaji wenzake wanaoshiriki Kombe la Mapinduzi.

Dabo ambaye naye ni raia wa Senegal, kabla ya kuja Tanzania aliwahi kufanya kazi na Sarr wakati anaichezea Klabu ya Teungueth ya Ligi Kuu nchini humo pamoja na Gibril Silla na Pape Ousamane Sakho.

Akizungumza visiwani Zanzibar, Dabo amesema usajili walioufanya Simba SC kwa kuinasa saini ya kiungo mkabaji, Sarr ni moja ya sajili bora kwa sababu ya kipaji kikubwa alichonacho kitakwenda kusaidia sana timu hiyo.

Amesema anafahamu uwezo na ubora wa nyota huyo, hivyo anaimani usajili huo utaongeza kitu kwenye nafasi ya kiungo na kuisaidia sana Simba SC, akishirikiana vema na wachezaji wenzake ndani ya timu hiyo.

“Sarr ni kijana wangu nilikuwa naye Teungueth miaka miwili iliyopita, ni kiungo mzuri na mchezaji bora anayejua kupambana, hapa Simba SC wamepata mtu na atawasaidia sana katika timu yao.

“Huu ni usajili bora kwao na nimefurahia kumuona ni sehemu ya soka la Tanzania, namkaribisha na nitamsaidia kuzoea mazingira si kwenye timu bali nchini kwa sababu nina baadhi ya taarifa ya baadhi ya maeneo,” amesema Dabo.

Ameongeza kabla ya kutua nchini amekuwa akiwasiliana naye kwa kipindi kirefu tangu alipokuwa nchini Tunisia, hivyo anaamini hii itakuwa nafasi yake ya kuonana naye tena.

Wakati huo huo Meneja wa Habari na Mawasiliano Simba SC, Ahmed Ally, alisema ujio wa kiungo huyo Utaenda kutibu matatizo yote ya kiulinzi ya timu yao.

Amesema miaka ya hivi karibuni wamekuwa wakikosa namba sita asilia, hivyo baada ya kutua kiungo huyo, wanaimani tatizo limetatulika, tangu alivyoondoka James Kotei, Gerson Fraga na Teddeo Lwanga, hawajapata kiungo asilia wa ukabaji.

“Tumepambana kupata saini ya kiungo Sarr, ni mchezaji tuliyemkosa katika timu yetu kwa muda mrefu, tumekuwa na wachezaji bora, lakini hatukuwa na namba sita asilia.

Sasa kati patakuwa na Sarr, Sadio Kanoute, Mzamiru Yassin na Abdallah Hamis, tutakuwa na safu bora sana ya kiungo,” amesema Ahmed.

Siku nane za maamuzi Mtibwa Sugar
Kocha Nigeria aahidi makubwa AFCON 2023