Siku nane zikisalia kabla ya Dirisha Dogo la usajili kufungwa Januari 16, mwaka huu, Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila, ameweka wazi juu ya nafasi anazotaka kuongeza nguvu ikieleza kuwa kipa, beki, kiungo na mshambuliaji.
Wakati Katwila akitaja nafasi hizo kuna taarifa kuwa kipa aliyetemwa na Coastal Union, Justine Ndikumana na kiungo wa Simba SC Nassor Kapama anayedaiwa huenda akatolewa kwa mkopo, tayari uongozi wa Mtibwa Sugar umeingia mawindoni kusaka saini zao.
Katwila amesema katika mapendekezo yake ametaka kuongezewa watu wanne katika nafasi hizo ili kuboresha kikosi cha timu kuelekea mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Amesema kulingana na mapendekezo yake, endapo atawapata wachezaji hao anaamini watafanya kazi nzuri na kuitoa timu hiyo katika nafasi ya chini waliopo kwa sasa katika msimamo wa ligi hiyo.
Kuhusu kuwasajili wachezaji hao wawili, Katwila amesema: “Siwezi kuzungumzia juu ya wachezaji hao kwa sababu bado hawajafika kambini, nilikabidhi mapendekezo kwa mtendaji mkuu wa timu kufanyia kazi. Kama tutapata huduma zao itakuwa vizuri kwa sababu watakuja kusaidia timu.
“Unajua suala la mkopo hadi mchezaji akubali kama atatolewa na kujiunga kwetu, ninaimani kubwa uongozi unafuata mapendekezo ambayo nimewapa ikiwamo kuboresha baadhi ya nafasi ninazohitaji kuimarisha timu yetu.”
Mtibwa Sugar ambayo imebakiza mchezo mmoja kabla ya kukamilisha mechi za mzunguko wa kwanza, inaburuza mkia katika msimamno wa ligi hiyo ikiwa na pointi nane baada kushinda mechi mbili tu na sare mbili huku ikiongoza kwa kuruhusu mabao mengi zaidi (29) hadi sasa.