Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Klabu ya Simba SC, Salim Abdallah ‘Try Again’ ameusifia usajili wa kiungo mpya wa timu hiyo, Msenegal, Babacar Sarr akitamba umekuja kumaliza tatizo la nafasi hiyo.
Msenegal huyo alitambulishwa juzi Jumamosi (Januari 06) mara baada ya kufikia makubaliano mazuri na Simba SC na kusaini mkataba wa miaka miwili ya kukipiga klabuni hapo katika dirisha hili dogo.
Ujio wa kiungo huyo umekuja kuwapa ugumu wa namba viungo Fabrice Ngoma, Sadio Kanoute na Mzamiru Yassin.
Try Again amesema kuwa ubora wa kiungo huyo wa kukaba na kuchezesha timu ndani ya wakati mmoja kumekuja kuiboresha nafasi hiyo kwa kiwango kikubwa kutokana na ubora alionao.
Salim amesema kuwa usajili wa kiungo huyo ni mapendekezo ya Kocha Mkuu wa timu hiyo Abdelhak Benchikha ambaye alimuona akiwa anaichezea US Monastir ya Morocco.
Ameongeza kuwa anaamini kiungo atakuja kumaliza tatizo la nafasi ya kiungo mkabaji, kutokana na kukidhi mahitaji ya kocha huyo mkutoka Algeria.
“Kabla ya kumsajili tulimfuatilia Sarr kwa karibu baada ya kocha wetu Benchikha kumpendekeza kabla ya kumsajili katika dirisha hili dogo lililofunguliwa.
“Sarr anakuja kuiboresha eneo la kiungo ambalo kocha alipendekeza kumsajili, hivyo kiungo huyo tunaamini ataifanyia makubwa Simba SC.
“Kiungo huyu ana vigezo vyote ambavyo kocha anavihitaji ambavyo ni kukaba na kuchezesha timu ndani ya wakati mmoja, hivyo Wanasimba wasubirie kupata burudani kutoka kwa Sarr ambaye amekuja kuongeza ushindani kwa viungo Ngoma, Kanoute na Mzamiru,” amesema Try Again.