Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali imeweka kipaumbele namba moja katika sekta ya elimu kwa kuongeza bajeti kutoka shilingi bilioni 265 mwaka 2021 hadi shilingi bilioni 457.
Dkt.Mwinyi ameyasema hayo mara baada ya kufungua Skuli ya kisasa ya Msingi Fuoni Wilaya ya Magharibi B, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Amesema, lengo ni kuongeza juhudi katika sekta hiyo kwa ujenzi wa miundombinu ya kisasa ikiwemo Skuli za msingi na Sekondari za ghorofa zinazojumuisha maabara za kisasa, maktaba na vyumba vya kompyuta.
Aidha, Rais Dkt.Mwinyi pia ameeleza kuwa Serikali itaendelea kuajiri walimu wa fani zote hususani wa masomo ya sayansi na hesabu ili waweze kutoa elimu bora na kwa mwaka huu itaajiri walimu 1,500.