Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi amemuagiza Mkandarasi anayetekeleza Miradi ya Maji ya Funta na Mradi wa Maji wa Wanga iliyopo Wilayani Lushoto Mkoani Tanga kuwa miradi hiyo iweze kukamilika kabla ya Aprili 30, 2024 huku akisema itakapofika muda huo hatapewa muda wa nyongeza.
Mhandisi Mahundi ametoa agizo hilo wakati alipotembelea na kukagua utekelezaji wa miradi hiyo miwili, kwenye Jimbo la uchaguzi Bumbuli lililopo Wilayani Lushoto
Amesema, “utekelezaji wa Mradi wa Maji Funta ulianza rasmi Agosti 18 2022 na ulipaswa kukamilika ndani ya siku 270 lakini mpaka sasa haujakamilika naomba nisisitize itakapofika April 30 hakutakuwa na kuda wa nyongeza tunahitaji wananchi 4782 wa maeneo ya Funta na Manga, na wananchi wa kijiji cha Manga na Kwemkole 2339 waweze kupata huduma.”
Aidha, Mhandisi Mahundi pia amewataka Wananchi kuendelea kutunza miundombinu ya maji pamoja na vyanzo vyake ili miradi inayotekelezwa iwe endelevu.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Kalist Lazaro ameahidi kumsimia kwa karibu Mkandarasi huyo ili miradi hiyo itekelezwe kwa wakati na wananchi waweze kupata huduma ya maji.
Mradi huo, unagharimu jumla ya Shilingi Milioni 832.6 na baada ya kukamilika unaenda kutatua changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi.
Aidha, ukamilika kwa miradi hiyo kunatarajia kunufaisha wananchi elfu 7121 wa Wilaya ya Lushoto katika kupata huduma ya maji safi na salama.