Rais wa Klabu Bingwa nchini Ufaransa Paris Saint-Germain, Nasser Al-Khelaifi, amethibitisha kuwa anataka Kylian Mbappe kubakia kwenye klabu hiyo zaidi ya msimu huu wa joto.
Mbappe ameingia miezi sita ya mwisho ya mkataba wake na yuko huru kwa mara nyingine tena kuzungumza na klabu yoyote, huku Real Madrid wakiongoza kwenye mbio za kuwania saini ya Mfaransa huyo.
Ripoti zinazodai Mbappe tayari amekubali kujiunga na Madrid zilikanushwa hivi majuzi na wawakilishi wa mshambuliaji huyo, hata hivyo, huku mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 akithibitisha hadharani kuwa bado hajafikia uamuzi.
Al-Khelaifi sasa ameapa kuendeleza pambano la kumbakiza Mbappe, akisisitiza kuwa angefurahi zaidi ikiwa atabaki Paris.
“Bila shaka nataka Kylian abaki, hilo ni la uhakika,” alisema Al-Khelaifi akiwaambia waandishi wa habari.
Yeye ndiye mchezaji bora zaidi duniani, na klabu bora zaidi kwa Kylian ni PSG. Yeye ndiye yupo katikati ya kila kitu.”
Wakati PSG wakiwa na matumaini ya kumbakisha Mbappe, wababe hao wa Ufaransa hawajali uwezekano wa kumpoteza kwa uhamisho wa bila malipo baada ya makubaliano na Mbappe majira ya joto yaliyopita ambayo yanalinda fedha zao.