Kocha Mkuu wa Simba SC, Abdelhak Benchikha ametoa onyo kali kwa wachezaji wa timu hiyo akiwataka kujitoa na kujituma kwa ajili ya kuipambania nembo ya klabu hiyo, na kuwawashia taa nyekundu wachezaji wavivu.
Benchikha amesema timu hiyo ina wachezaji wenye vipaji na uwezo mkubwa lakini baadhi yao wametawaliwa na uvivu wa mazoezi na kujituma uwanjani.
“Kuna wachezaji wana uwezo mkubwa na vipaji, lakini tatizo linakuja kwenye kujituma na kuipambania timu, kama kocha siwezi kuvumilia hali hii na nimewaambia wabadilike,” amesema Benchikha.
Aidha, amesema hataweza kuvumilia kuona mchezaji anacheza chini ya kiwango kwa sababu atakuwa anakwamisha mipango yake na kile kinachotarajiwa na Wanasimba na wadau wa soka nchini.
Benchikha ametoa kauli hiyo kufuatia kuwapo kwa sakata la kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Clatous Chama kupelekea kusimamishwa kwa madai ya utovu wa nidhamu na kupelekwa kwenye kamati ya nidhamu ndani ya timu hiyo.
Simba SC ipo visiwani Zanzibar katika mashindano ya Kombe la Mapinduzi ambapo Benchikha anayatumia kuandaa timu yake kwa ajili ya michezo ijayo ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi.
Kocha huyo anatumia mashindano ya Mapinduzi pia kutengeneza muunganiko na kombinesheni ya wachezaji wapya waliosajiliwa katika kipindi hiki cha dirisha dogo.
Simba SC imewasajili Ladack Chasambi kutoka Mtibwa Sugar, Saleh Karabaka kutoka JKU FC ya Zanzibar na Babacar Sarr raia wa Senegal.
Benchikha amesema kuwa wachezaji wake wote wanapaswa kuwa kwenye daraja moja ambao wanatakiwa kuhakikisha wanajituma ndani ya timu yao na wala hataki kusikia kuna mchezaji mkubwa kuliko timu yenyewe.
“Sihitaji kuona mchezaji anajiona mkubwa kuliko timu jambo ambalo litaharibu na kuleta mvurugano kwa walio kwenye mstari wa timu, nataka kuona kila mchezaji anatimiza wajibu wake ili kufikia malengo yetu hasa kwenye ligi na michuano ya kimataifa, sitamvumilia mchezaji atakayeenda kinyume na hili,” amesema Benchikha.