Mabosi wa Manchester City wanaamini Mshambuliaji wao Erling Haaland anaishi kwa furaha, hivyo hatakuwa na mpango wa kuachana na timu hiyo yenye maskani yake Etihad hivi karibuni.
Ripoti kutoka Hispania zilifichua kuwa Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Norway yupo kwenye mipango ya kutimkia zake Real Madrid muda wowote kuanzia sasa.
Na imeelezwa kwamba hata kwenye mkataba wa mchezaji huyo kuna kipengele kinachohitaji kuulipia Pauni 85 milioni tu ili kutimkia zake Bernabeu.
Hata hivyo, hilo haliwapi presha Man City juu ya kumpoteza kinara wao wa mabao, ambaye amekuwa kwenye kiwango matata kabisa kwa kipindi cha miezi 18 aliyokuwa kwenye soka la England.
Los Blancos pia inafikiria kumnasa Kylian Mbappe kwa uhamisho wa bure mwishoni mwa msimu huu wakati mkataba wake utakapofika tamati huko Paris Saint-Germain.
Man City inachofikiria kwa sasa ni kumpa Haaland mkataba mpya ambao utamfanya kuwa mchezaji anayelipwa mshahara mkubwa zaidi kwenye Ligi Kuu England.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 23, amekuwa moto tangu alipotua kwenye Ligi Kuu England, ambapo amefunga mabao 71 kuanzia majira ya kiangazi 2022 aliposaini mkataba wa miaka mitano ya kutumikia miamba hiyo ya Etihad.
Kinachoibua wasiwasi ni ripoti ya kwamba Haaland ana nyumba huko Hispania, kitu ambacho kinaweza kumvutia na kwenda kukipiga huko Real Madrid.