Mfungaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ya 2016/17, Abdurahman Mussa amesajiliwa na klabu ya Mashujaa FC siku chache kabla ya kufungwa kwa dirisha dogo la usajili.
Taarifa iliyotolewa na klabu hiyo inasema kuwa wamemsajili mchezaji huyo kwa ajili ya kuongeza nguvu katika nafasi ya ushambuliaji.
Klabu hiyo imesema hivi sasa ipo kwenye maboresho katika kipindi hiki ili kuhakikisha si tu kwamba inabaki Ligi Kuu, lakini pia kuwapa burudani mashabiki wa soka mkoani Kigoma.
Kocha Mkuu Mohamed Abdallah ‘Bares,’ amesema anaamini usajili anaofanya kwa sasa utakuwa na tija na kuifanya timu hiyo kuwa bora zaidi.
“Tunasajili maeneo ambayo tunaona kuna mapungufu, naamini usajili ni mzuri na tutakuwa na timu imara,” amesema Bares.
Abdurahman alikuwa mchezaji wa Ruvu Shooting ambayo kwa sasa inaitwa JKT Tanzania na alishawahi kuwa mfungaji bora msimu wa 2016/17 akiwa sawa na Simon Msuva, wote wakipachika mabao 14.
Wakati huo Msuva alikuwa kwenye klabu ya Young Africans kabla ya kwenda kucheza soka la kulipwa nchini Morocco kwenye klabu ya Difaa El Jadida mara baada ya ligi ya msimu huo kumalizika.
Mashujaa FC imeshafanya usajili wa wachezaji kadhaa kipindi hiki cha Dirisha Dogo, ikiwa tayari imeshawasainisha wachezaji, Emmanuel Mtumbuka kutoka Stand United ambaye ni Mshambuliaji, Winga Nyeyezi Juma kutoka Inter Star ya Burundi pamoja na kiungo Balama Mapinduzi kutoka Coastal Union.