Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amefanya ziara Makao makuu ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya – DCEA, jijini Dar es Salaam na kuipongeza kwa ukamataji wa dawa za kulevya zaidi ya Tani 3.

Akizungumza na Maafisa wa DCEA, Majaliwa, amesema Serikali inathamini kazi kubwa inayofanywa na mamlaka hiyo katika kupambana na dawa za kulevya, huku akidai kuwa, kukamatwa kwa dawa hizo ni ushindi mkubwa katika vita dhidi ya dawa za kulevya.

Alisema, ‘‘nimekuja kuona mwenyewe zile dawa mlizokamata… lakini pia kuwapongeza kwa kazi nzuri mliyoifanya, mafanikio haya yanaanza kuleta sura ya kwamba Tanzania si mahali sahihi kwa kuzalisha, kusafirisha, kuuza na sio mahali pazuri kwa Matumizi ya Dawa za kulevya.’’

Aidha, Majaliwa ameitaka DCEA kuendelea kufanya kazi kwa bidii, ili kuhakikisha kuwa dawa za kulevya zinatokomezwa nchini, huku akiahidi kuwa, Serikali itaendelea kuiwezesha mamlaka hiyo, ili iweze kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

“Nawaomba Mamlaka muendelee kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha kuwa dawa za kulevya zinatokomezwa nchini na sisi kama Serikali tutaendelea kuiwezesha mamlaka hii ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi,”ameongeza Majaliwa.

Kwa upande wake Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Aretas Lyimo, amemshukuru Waziri Majaliwa na serikali kwa ujumla, chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuiwezesha Mamlaka kufanikisha kazi zake.

‘‘Naomba kukushuru wewe Mhe. Waziri Mkuu kwa kuendelea kuisimamia mamlaka katika kutekeleza kazi zake vizuri chini ya maelekezo na maagizo yako, ambayo unayatoa mara kwa mara kupitia kwa wasaidizi wako na sisi kama watumishi tunahakikisha tunatekeleza maagizo yako kwa weledi na ufanisi mkubwa, ili kuhakikisha malengo ya Tanzania bila dawa za kulevya inawezekana na kuwa salama,” amesema Lyimo.

Desemba mwaka jana, DCEA ilikamata dawa za kulevya zaidi ya tani 3 katika eneo la Kibada, Dar es Salaam, dawa hizo ni aina ya Heroin na Methamphetamine, ambapo kiwango cha dawa hizo za kulevya ni kikubwa ambacho hakiwaji kukamatwa nchini tangu shughuli za udhibiti zianze kufanyika.

Mfungaji bora Ligi Kuu atua Mashujaa FC
Real Madrid yahusishwa na Erling Haaland