Baada ya kuonesha uwezo mkubwa kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi 2024, kiasi cha kuwabadili mawazo mabosi wa klabu hiyo waliokuwa mbioni kumtema, beki wa kati wa Young Africans, raia wa Uganda, Gift Fred amesema sasa anaitaka Ligi Kuu Bara kwani ndiko kulichomleta nchini.
Gift aliyesajiliwa msimu huu akitokea Sports Club Villa ya Uganda ameshindwa kupenya kikosi cha kwanza cha Young Africans, lakini ametumika kwenye michuano ya Mapinduzi na kuonyesha uwezo mkubwa kiasi cha kuwafanya mashabiki kushangazwa naye.
Beki huyo anayecheza nafasi moja na mabeki walipo timu ya taifa, Taifa Stars, Dickson Job, Bakari Mwamnyeto na Ibrahim Bacca amesema kwa sasa anataka apewe nafasi katika mechi za ligi kwani anaamini huko ndiko anakotakiwa kuipigania timu.
Akizungumza akiwa mapumzikoni nchini Uganda, Gift amesema licha ya kukaa kwake nje kwa muda mrefu bado ana matumaini ya kuwa ipo siku atafanya makubwa katika ligi.
Amesema lazima atimize kilichomleta tena kwa kiwango bora licha ya wachezaji aliowanao ndani ya Young Africans kuweka ushindani mkubwa wa namba, ila nafasi yake bado anaiona na ana uhakika wa kufikia malengo.
“Kutokupata nafasi ya kucheza wala sio shida ingawa sio sawa kwa mchezaji, ila kikubwa ni kujiamini na kuhakikisha unamuonyesha kocha kuwa hakufanya makosa kukupanga katika mechi atakayokupa.
“Mimi naitaka ligi ili niweze kufanya makubwa huko, kwani hadi nafika Young Africans maana yake nina uwezo hivyo ninahamisha nguvu huko.”