Mbunge wa Jimbo la Kwela Mkoani Rukwa na Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge inayoshughulikia uwekezaji wa Mitaji ya Umma, Deus Sangu, amesema historia imeandikwa kutokana na watu wengi kutoa maoni ya muswada wa Uwekezaji wa Mitaji ya Umma.
Akizungumza Jijini Dodoma, Sangu amesema kwa mara ya kwanza Novemba 10, 2023 Serikali kupitia Bunge walipeleka muswaada huo ili kuleta mabadiliko na mageuzi kwenye sekta ya uchumi na kufanya marekebisho hasa kwenye Ofisi ya Msajili Mkuu wa Hazina.
“Ofisi ya msajili wa hazina kwa majukumu yake pamoja na mambo mengine ilikuwa ni kama ofisi ambayo inasimamia mashirika ya umma, lakini kwa muda mrefu sana tangia kuanzishwa kwa ofisi ya msajili wa hazina kumekuwa na gepu kubwa kwenye huendeshaji wa mashirika ya umma.” alisema.
Sangu aliongeza kuwa, “tuna mashirika mengi ambayo kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na msajili wa hazina mpaka kufikia June mwaka jana yalikuwa 304, mwanzo yalikuwa 298 lakini kutokana na uwekezaji ambao serikali imekuwa ikiendelea kufanya yameongezeka mpaka kufikia hapo.”
Hata hivyo, amesema takwimu za mwezi Juni 3023 zinaonesha uwekezaji katika Mashirika hayo bado upo chini na Serikali imewekeza zaidi ya Tirioni 76.73 na kukua hadi Tirioni 80 na wanakisudia kufikia Trilioni 100.