Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria imeendelea utekelezaji wa kampeni ya kutoa huduma ya Msaada wa Kisheria bure kwa Wananchi ‘Mama Samia Legal Aid Campaign’ katika Mkoa wa Singida ambapo Wananchi wengi wamejitokeza kuchangamkia fursa hiyo.
Wakili wa Serikali kutoka Wizara ya Katiba na Sheria ambaye pia ni Kiongozi wa timu ya msaada wa kisheria iliyopo Manispaa ya Singida, Athuman Msosole amesema wameanza kampeni hiyo kwa kutoa elimu ya msaada wa kisheria kwa kutembelea kata ya Mtamaa ambapo wamefanikiwa kufika katika Vijiji vitatu pamoja na kukutana na Wanafunzi wa shule ya Mtamaa, ambao wamepatiwa elimu ya masuala mbalimbali ikiwemo ya ukatili wa Kijinsia.
“leo ni siku ya kwanza mwitikio umekuwa wa kuridhisha, kwa sababu tumepata idadi kubwa ya akina Mama ambao walifika kwa wingi na kuuliza maswali mbalimbali baada ya uwasilishaji wa mada kutoka kwa Wataalam wetu, siku ya kesho Ijumaa tutakuwa katika maeneo mengine ambayo tunategemea kuwa na mwitikio mkubwa zaidi,’’ameeleza.
Amesema lengo la kampeni hiyo ni kutoa msaada wa elimu ya kisheria kwa Wananchi, na kutatua migogoro mbalimbali ikiwemo ya ardhi, ndoa, mirathi na matunzo ya Watoto; hivyo amewataka Wananchi kujitokeza kwa wingi kuchangamkia fursa hiyo katika maeneo yote ambayo huduma hiyo inapatikana mpaka kufikia tarehe 19 Januari 2024.
Kampeni hiyo inatokana na Azma ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye anataka kuona Tanzania inaendelea kuwa nchi tulivu na yenye amani kwa kuwawezesha Wananchi sio tu kupata msaada wa kisheria bali kuwaelimisha kuhusu haki zao na wajibu wao kwa Taifa, Kila mmoja wetu akifahamu vizuri haki zake na wajibu wake, ndipo nchi yetu itasonga mbele kiuchumi.