Kocha wa Mali Eric Chelle amesema kuwa timu yake inatafuta heshima katika mashindano ya Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’ yanayoendelea nchini Ivory Coast, ikianzia dhidi ya Afrika Kusini katika mchezo wa Kundi E.
Mchezo huo utafanyika kwenye Uwanja wa Amadou Gon Coulibaly huko Korhogo leo Jumanne (Januari 16).
Mali inakwenda katika mchezo huo baada ya kushinda mabao 6-2 dhidi ya timu ya Guinea-Bissau, mwishoni mwa juma lililopita katika mchezo wa kujipima nguvu, matokeo ambayo yanafuatia mechi mbili za kufuzu kwa Kombe la Dunia zilizofanyika Novemba.
Katika mechi hizo, Mali ilishinda kwa mabao 3-1 dhidi ya Chad na kutoka sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Afrika Kusini wenyewe wakati wa maandalizi ya ‘AFCON 2023’ walitoka suluhu dhidi ya Lesotho Jumatano ya juma lililopita.
Bafana Bafana nayo pia ilikuwa katika mechi za kufuzu kwa Kombe la Dunia Novemba mwaka jana, ikishinda 2-1 dhidi ya Benin na kufuatia na kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Rwanda.
Habari za timu Kikosi cha timu ya taifa ya Mali hakina majeruhi na kitakuwa imara kwa ajili ya mchezo huo, huku Afrika Kusini wenyewe wakitarajia kurejea kwa wachezaji wake wawili, Ronwen Williams na Themba Zwane, baada ya kukosa mchezo dhidi ya Lesotho kutokana na majeruhi.