Wakati Uongozi wa Klabu ya Young Africans ukisema umesikia kilio cha mashabiki wao kuhusu kuimarisha safu yao ya ushambuliaji na umeshusha mshambuliaji mwenye uwezo wa hali ya juu katika kipindi hiki cha dirisha dogo lililofungwa jana usiku, pia umetangaza kuachana na winga wao, Jesus Moloko kwa makubaliano ya pande zote mbili.

Joseph Guédé Gnadou ambaye amesajiliwa kabla ya dirisha la usajili kufungwa jana usiku, alitambulishwa usiku wa manane kama ilivyokuwa kwa kiungo mshambuliaji, Stephane Aziz Ki mwaka 2022.

Tayari Young Africans ilifanya usajili wa dirisha dogo kwa kutambulisha nyota wawili, Shekhan lbrahim kutoka JKU FC ya visiwani Zanzibar na Augustine Okrah aliyewahi kuitumikia Simba SC msimu uliopita.

Ofisa Habari wa Young Africans, Ali Kamwe, amesema wamefanya mabadiliko machache kwa kufuata mapendekezo ya Kocha Mkuu, Miguel Gamondi, kwa kuimarisha safu ya ushambuliaji.

Amesema wamesikia kilio cha benchi la ufundi na mashabiki wa timu hiyo kuhakikisha katika usajili huu wanaimarisha safu ya ushambuliaji kwa kuleta mtu hatari.

“Ni kweli tumefanya kazi tuliyotumwa na kusikililiza kilio cha kocha Gamondi pamoja na mashabiki wetu juu ya kusajili mshambuliaji, tayari tumeshakamilisha usajili wake na atakuwa sehemu ya kikosi cha timu yetu kipindi chote cha mkataba wake,” amesema Kamwe.

Ameeleza kuwa tayari kuna baadhi ya wachezaji wametolewa kWa mkopo kulingana na mapendekezo ya kocha Gamondi na kupisha usajili mpya.

Katika hatua nyingine umeweka wazi kuachana na winga Mkongomani, Moloko kwa makubali ya pande zote mbili, Young Africans imefikia hatua hiyo baada ya nyota huyo kukosa nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha Kocha Miguel Gamondi.

Moloko alikuwa kwenye kikosi cha Young Africans kilichoshiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi 2024 na kutolewa hatua ya Robo Fainali kwa kipigo cha mabao 1-3 dhidi ya APR FC.

Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Young Africans, Ali Kamwe, wamechukua maamuuzi ya kuachana na winga huyo kutokana na makubaliano ya pande zote mbili ili kupisha nafasi ya usajili mpya kuingia.

Wachezaji Simba SC wapewa saa sita
Eric Chelle: Tunasaka heshima AFCON 2023