Kocha Mkuu wa Simba SC, Abdelhak Benchikha amewapa mapumziko ya siku 10 wachezaji wake ambapo watarejea kambini Januari 24, mwaka huu, kujiandaa na mechi mbalimbali za mashindano huku wakiondoka na programu ya saa sita kwa siku.

Mapumziko ya wachezaji hao yalianza mara baada ya kurejea kutoka Zanzibar ambako timu hiyo ilikuwa inashiriki mashindano ya Kombe la Mapinduzi.

Katika mashindano hayo, Simba SC ilikuwa mshindi wa pili huku Mlandege ikitetea kombe hilo kwa ushindi wa bao 1-0 katika mchezo uliochezwa Jumamosi (Januari 13) kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Unguja.

Simba SC ikirudi kambini itakuwa na kibarua cha kujiandaa na mechi za Ligi Kuu Bara, hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika pamoja na Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’

Miongoni mwa mechi ambazo huenda Simba SC ikaanza nazo ligi itakaporejea baada ya kumalizika kwa michuano ya AFCON 2023 inayoendelea nchini lvory Coast ni zile za viporo dhidi ya Azam FC, Mashujaa na Geita Gold FC.

Simba SC ina mastaa watano kwenye timu ya taifa ‘Taifa Stars’ ambao wataungana na kikosi chao baada ya ‘AFCON 2023’. Nyota hao ni Kibu Denis, Mzamiru Yassin, Aishi Manula, Mohamed Hussein Tshabalala’, Clatous Chama na Henock Inonga.

Mmoja wa viongozi wa Benchi la Ufundi wa timu hiyo ambaye aliomba hifadhi ya jina lake amesema kuwa kila mchezajj amepewa programu ya kufanya.

“Kila mchezaji amepewa programu yake, kocha atafuatilia hatua kwa hatua maana hawawezi kukaa bila mazoezi kwa siku zote hizo, wanapumzika lakini watakuwa na kitu cha kufanya, nafikiri kila siku mchezaji atakuwa na programu ya saa sita.”

Tuchel: Rekodi iko hatarini
Moloko apishana na mshambuliaji Young Africans