Kocha Mkuu wa Ajax, John vant Schip, amethibitisha nia ya klabu hiyo kutaka kumsajili nahodha wa zamani wa Liverpool, Jordan Henderson.
Vyanzo viliiambia ESPN mapema juma hili kwamba Henderson, ambaye hana furaha kule Saudi Arabia, anasakwa na Ajax pamoja na timu za Ligi Kuu England na Ligi Kuu ya Ujerumani, Bundesliga.
Akizungumza kabla ya mechi ya Ligi Kuu Uholanzi ‘Eredivisie’ dhidi ya Go Ahead Eagles, Vant Schip aliiambia ESPN kwamba mazungumzo yanaendelea kuhusu uhamisho huo.
“Kuna mazungunzo mazito yanaendelea na Henderson, alisema Vant Schip. Bado ana baadhi ya mambo ya kupanga huko Saudi Arabia.”
“Si siri kwamba tunaweza kumtumia mchezaji wa aina hiyo. Vijana wengine wanaweza kufaidika kwa hilo.”
Lakini chanzo kiliiambia ESPN kwamba, Al Ettifaq inaweza kutokuwa na nia ya kumruhusu kiungo huyo mkongwe kuondoka miezi michache tu baada ya kumsajili.
Henderson mwenye umri wa miaka 33, alihamia Saudi Pro League kutoka Liverpool Julai 2023, na kumaliza kukaa kwa miaka 12 pale Anfield na kumfanya kushinda Ligi Kuu England, Ligi ya Mabingwa Ulaya, Kombe la FA, UEFA Super Cup na Kombe la Klabu Bingwa Dunia.
Hata hivyo, Al Ettifaq wanasita kumwona mchezaji huyo wa Kimataifa wa England akiondoka kwani inaweza kuathiri sifa si tu ya klabu bali hata ligi.
Ajax wako tayari kulipa ada ndogo ya uhamisho, lakini hawana nia ya uhamisho wa mkopo, chanzo kiliiambia ESPN.