Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Damas Ndumbaro amefanya mazungumzo maalumu na kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) kilichoweka kambi katika mji wa San-Pedro nchini Ivory Coast kujiandaa na mchezo wa kwanza wa #AFCON2023, dhidi ya Morocco.
Dkt. Ndumbaro amezungumza na wachezaji hao mara baada ya kushuhudia mazoezi na utayari wa kikosi hicho kuelekea mchezo wao wa kesho dhidi ya Morocco utakaopigwa mjini humo.
Baada ya mazungumzo yaliyodumu kwa takribani saa mbili, Dkt. Ndumbaro amesema ameridhishwa na maandalizi ya kikosi hicho, ari na morali ya wachezaji na benchi la ufundi ambayo inatoa picha nzuri ya kufanya vema katika kundi “F”.
Kikao hicho kimehudhuriwa pia na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF) ambaye pia ni Mkuu wa msafara wa timu Suleiman Mahamoud Jabir.