Uongozi wa Beki wa kushoto wa Young Africans raia wa DR Congo, Joyce Lomalisa Mutambala umefikia makubaliano mazuri ya kuongeza mkataba mwigine wa mwaka mmoja na nusu wa kuendelea kukipiga klabuni hapo.
Lomalisa ambaye anasifika kwa kupiga krosi safi ‘Kumwaga Maji’, alibakiza miezi sita katika mkataba wake ambao ulikuwa unamalizika mwishoni mwa msimu huu.
Beki huyo alirejea hivi karibuni katika la Michuano ya Kombe la Mapinduzi akitokea katika majeraha ya enka aliyoyapata katika mchezo wa Makundi wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Al Ahly ya nchini Misri.
Mmoja vwa Mabosi wa Young Africans kutoka ndani ya Kamati ya Mashindano ya timu hiyo, amesema kuwa, beki huyo ameongezewa mkataba wa mwaka mmoja wenye ofa kubwa uliomshawishi kusaini tena.
Bosi huyo ameongeza kuwa, beki huyo amekubali kusaini baada ya kumboreshea baadhi ya mahitaji yake aliyoyahitaji, ikiwemo mshahara na dau la usajili alilohitaji kwa viongozi hao kabla ya kusaini mbele ya meneja wake anayemsimamia.
Ameongeza kuwa uwezo na uzoefu wa kucheza Ligi ya Mabingwa Barani Afrika na Ligi Kuu Tanzania Bara, ndiyo umemshawishi Kocha Mkuu wa timu hiyo, Muargentina Miguel Gamondi kupendekeza kumbakiza Young Africans.
“Kabla ya dirisha kufungwa usiku wa kuamkia jana Jumanne (Januari 16), viongozi wetu wa Young Africans na meneja wa Lomaisa tulikutana na kumpa ofa yetu na yeye kutupa yake na kufanya maamuzi ya kumuongezea mwingine.
“Makubaliano hayo yalifikia sehemu nzuri na kufikia makubaliano mazuri ya kumuongezea mkataba mnono ambao yeye mwenyewe mchezaji na meneja wake wameridhika na kusaini.
“Ni mkataba wa mwaka mmoja pekee aliousaini, hivyo atakuwa na mwaka mmoja na nusu wa kubakia Young Africans, kwani alibakiza miezi sita,” amesea bosi huyo.
Rais wa Young Africans Injinia Hersi Said amezungumzia hilo kwa kusema kuwa: “Tunatengeneza timu itakayokuwa bora na tishio katika Ukanda huu wa Afrika, hivyo hatutamuchia mchezaji yeyote aliyokuwepo katika mipango ya kocha wetu.”