Afarah Suleiman, Simanjiro – Manyara.
Mkuu wa Mkoa Manyara, Queen Sendiga akiwa katika kijiji cha Kimotoron Wilayani Simanjiro ametatua mgogoro kati ya Wananchi wa Kijiji hicho na Hifadhi ya Taifa ya Tarangire, uliopelekea Askari wa hifadhi hiyo kushikilia mifugo na watu wanane na kuamuru kuachiwa kwa Mifugo hiyo zaidi ya 800.
Sendiga ametoa agizo hilo la kuachiwa kwa mifugo hiyo ikiwemo Ng’ombe, Mbuzi na Kondoo iliyokua inashikiliwa na Uongozi wa Hifadhi, baada ya wafugaji kuingiza mifugo hifadhini na kuwataka kuacha kutumia nguvu na kuwapiga Wananchi, badala yake panapo tokea jambo kama hilo wakae chini na kuzungumza kwa kuwa Tanznia ni nchi ya amani.
Aidha, amewaagiza viongozi wa ngazi mbalimbali kusimamia makubaliano na maelekezo ambayo yanapitishwa na Serikali au vikao na kuwaambia Wananchi ukweli pasipo kuwaficha, ili wapate uelewa juu ya maamuzi na maelekezo mbalimbali yanayotolewa na kuepusha migogoro isiyo na tija.
Sendiga pia ametoa maelekezo kwa uongozi wa hifadhi ya Tarangire kuwaacha Wananchi waendelee kupata huduma za mifugo yao ambazo bado zinapatikana katika hifadhi kama vile sehemu za kunyweshea mifugo na kuwataka Wananchi hao kuendelea kutii sheria, taratibu na kanuni zilizowekwa na kwamba wahifadhi wajizatiti katika utoaji wa elimu na kuboresha mahusiano kati yao na Wananchi.
Sambamba na hilo RC Sendiga amewajulisha Wananchi wa Kimotorok kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametoa kiasi cha shilingi Milioni 300, kwajili ya uboreshaji wa Miundombinu ya Elimu na Afya kijijini humo.