TIMU ya Taifa ya ngumi inatarajia kujipima ubavu na mabondia kutoka Kenya, Uganda, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Rais wa Shirikisho la Ngumi Tanzania (BF), Lukole Wililo, amesema mapambano hayo yanatarajiwa kuchezwa mwezi ujao jijini Dar es salaam.

Wililo amesema lengo la mapambano hayo ni kuipima timu ya taifa ambayo inajiandaa na mashindano ya kufuzu Olimpiki yatakayofanyika jijini Paris, Ufaransa, mwaka huu.

Amesema mapambano hayo yatawawezesha wanamasumbwi wa Tanzania kuongeza viwango, kubadilishana ujuzi na mabondia kutoka katika nchi ambazo nazo zinashiriki michuano ya Afrika na kufuzu Olimpiki.

Kiongozi huyo amesema kwa sasa mabondia wanafanya mazoezi ya kwenda na kurudi, katika klabu ya Mgulani JKT kabla ya kuingia kambini kucheza na mabondia wa nchi zilizotajwa.

Timu ya taifa inaundwa na mabondia 28, wanaume ni Abdulrazaq Hamisi Abdallah Mohamed, Azizi Waziri, Mwalami Mohamned, John Dominick, Hassani Mrutu, Shaibu Baruti, Lucas Majobanga, Abdallah Nachoka na Elias Damson.

Wengine Joseph Kasi, Alphonce Abel, llankunda Nkundabanyanka, Yusuph Changalawe, Mussa Malegesi, Matonyinga Kasala, Mhina Richard na Alex Mpini.

Wanamasumbwi wanawake ni Miriam Maligisa, Saraphina Fussi, Umukuruthum Mkumbi, Zulfa Macho, Aisha Hamisi , Latifa Uloki, Vumilia Kalinga, Leila Yazidu, Beatrice Nyambega na Grace Mwakamele.

MAKALA: Nsala Di Wala jasiri aliyewashangaza Wazungu
Hii hapa mashine mpya ya Dodoma Jiji FC