Mlinda Lango chaguo la kwanza katika kikosi cha Cameroon, Andre Onana ameweka wazi kuwa kocha wake, Rigobert Song alimwambia wazi kama atacheza mchezo wa Premier League dhidi ya Tottenham hatompanga kwenye kikosi chake kilichopambana dhidi ya Guinea, katika fainali za Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’ zinazoendelea nchini Ivory Coast.
Onana ambaye pia ni Mlinda Lango chaguo la kwanza Manchester United aliichezea klabu hiyo mchezo wa Premier Jumapili (Januari 14) dhidi ya Tottenham na kumalizika kwa sare ya mabao 2-2 na baada ya hapo akapanda ndege kujiunga na timu ya Taifa ya Cameroon kwenye michuano ya ‘AFCON 2023’.
Hata hivyo, Onana hakuwa sehemu ya kikosi cha Cameroon kilichocheza dhidi ya Guinea juzi Jumatatu (Januari 15) na mchezo kuisha sare ya bao 1-1.
Akizungumza baada ya kudaiwa alikasirika huku picha zikiomuonyesha akiwa amesimama koridoni na baaadhi kudai amekasirishwa kutopangwa kwenye mchezo huo wa kwanza, Onana alisema: “Ninayo mengi sana ya kuongea kwa sasa ila nimechagua kukaa kimya kwa heshima ya timu yangu ya taifa na mpira wa Afika kwa ujumla.
“Kocha alishaniambia mapema nikicheza mechi dhidi ya Spurs hatonipanga katika mchezo wa kwanza wa AFCON 2023, nililiheshimu hilo kwa sababu mwenye kipaji cha kukaa golini kwetu sio mimi pekee, wapo vijana kama Ondoa na ndio nilitamnani wapangwe katika mchezo huo, endapo nikikosekana na ikawa hivyo.
“Mtu anapiga picha nikiwa koridoni naongea mambo ya kimpira na malegend kadhaa wa soka la Afrika, halafu unaweka mitandaoni na kusema nilikuwa nimekasirika kisa sijapangwa kwenye mchezo, hii sio sawa.”