Kiungo wa Klabu ya Fulham, Alex Iwobi ameahidi kuwa timu ya taifa ya Nigeria ‘Super Eagles’ itakabiliana na Ivory Coast wakijiamini katika mchezo wao wa pili wa hatua ya makundi wa Kombe la Mataifa ya Afrika ‘AFCON 2023’.
Iwobi ameyasema hayo wakati akizungumzana vyombo vya habari kuhusu mchezo wao ujao dhidi ya wenyeji Ivory Coast baada ya timu hiyo kutoka sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya Guinea ya Ikweta katika mchezo wa ufunguzi wa Kundi A.
Iban Salvador aliiweka Guinea ya Ikweta mbele na matokeo kuwa 1-0 katika dakika ya 36 baada ya kupata mpira kutoka kwa Jose Machin aliyefanya kazi nzuri ya kuwatoka mabeki wa Nigeria.
Hata hivyo, uongozi huo ulidumu kwa dakika mbili tu, ingawa, mshambuliaji wa SSC Napoli, Victor Osimhen, ambaye awali alikuwa mchoyo baada ya kutoa pasi akaamua kupiga mwenyewe akitaka kufunga, lakini shuti lake lilipaa juu.
Super Eagles walifanikiwa kusawazisha na matokeo kuwa 1-1 wakati mshambuliaji wa Atalanta, Ademola Lookman, alipopiga krosi iliyomkuta Osimhen, aliyeachwa peke yake na kupiga mpira katika wavu usio na mlinzi na kuujaza mpira wavuni.
Nigeria mara kadhaa walikaribia kufanya matokeo kuwa 2-1, lakini walishindwa kufunga, na sasa wana kibarua dhidi ya wenyeji Ivory Coast, ambao waliifunga Guinea-Bissau kwa mabao 2-0.