Timu ya taifa ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), leo Jumatano (Januari 17) itashuka dimbani kupepetana Zambia katika mchezo wa kwanza wa Kundi F, katika michuano ya Kombe la Mataifa Afrika ‘AFCON 2023’, mechi itakayopigwa Uwanja wa Laurent Pokou, nchini Ivory Coast.
DRC itaingia dimbani huku ikipewa nafasi ya kufanya vizuri zaidi msimu huu, kutokana na ubora wa kikosi chake.
Timu hiyo iliwahi kutwaa ubingwa wa AFCON mara mbili ikiwa ni mwaka 1968 na mwaka 1974.
Hata hivyo, timu hiyo ilishindwa kufanya vizuri katika misimu mitatu baada ya kutolewa katika hatua ya makundi ikiwemo mwaka 2000 huku ikishindwa kufuzu mara tatu kati ya mwaka 2008 na 2012.
Katika michezo ya kufuzu fainali za msimu huu, DRC ilipoteza mechi mbili na kusababisha kutimuliwa aliyekuwa kocha wake, Hector Cuper.
Kocha Sebastien Desabre alikabidhiwa mikoba ya kuinoa timu hiyo na kufanikiwa kufuzu fainali hizo zinazoendelea nchini Ivory Coast.
Tangu mwaka 2005, timu hizo zimekutana mara tatu ambapo Zambia ilishinda mechi moja na kutoka sare michezo miwili.
Zambia iliwahi kutwaa taji hilo mwaka 2012 lakini misimu miwili baadae iliondolewa katika hatua ya makundi.
Timu hiyo hivi sasa ipo chini ya Kocha wa zamani wa Chelsea, Avram Grant, ambaye anapewa nafasi ya kukiongoza kikosi chake kufanya vyema.
Kocha Grant tayari alishaingoza Zambia kutwaa Kombe la COSAFA mwaka 2023 baada ya kuichapa Lesotho bao 1-0, huku akiiongoza timu hiyo katika mechi sita na kushinda michezo miwili, ilitoka sare mara mbili na kupoteza mara mbili.