Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC Ahmed Ally, anatamani Mashindano ya Kombe la Mataifa Afrika ‘AFCON 2023’ yamalizike hata leo ili waanze kuona ubora wa washambuliaji wao wapya, waliowasajili kabla ya dirisha dogo kufungwa la msimu huu.
Simba juzi Jumatatu (Januari 15) iliwatangaza washambuliaji wawili Fredy Michael Koublane na Pa Omar Jobe, ambao wametambulishwa saa chache kabla ya usajili kufungwa usiku wa kuamkia jana Jumanne (Januari 16).
Wakiwasajili nyota hao, haraka walitangaza kuachana na washambuliaji wake Moses Phiri na Jeane Baleke aliyerejeshwa katika klabu yake ya TP Mazembe ya DR Congo.
Ahmed amesema kuwa washambuliaji hao wote waliowasajili ni mapendekezo ya kocha wao Mualgeria, Abdelhak Benchikha ambao anafahamu ubora wao kabla ya kuwapa mikataba ya kuichezeat timu hiyo.
Amesema kuwa wao viongozi wanatamani mashindano ya AFCON 2023 imalizike mapema, kwa lengo la mashabiki kupata burudani ya mabao mazuri yatakayofungwa na washambuliaji hao wenye viwango bora.
Ameongeza kuwa mabeki wa timu pinzani wajiandae kupata ushindani mkubwa kutoka kwa washambuliaji hao, huku akiwataka mashabiki kujiandaa kushangilia mabao hadi wachoke wenyewe.
“Hizi mashine mbili tulizozitambulisha saa chache kabla ya dirisha dogo kufungwa, zinajua kufunga mabao hatari ambao mabeki watakuwa dhaifu, basi watakiona.
“Hiyo inatupa ujasiri wa kutamani AFCON 2023 imalizie hata leo, ili mashabiki wapate burudani ya kushangilia mabao watakayoyafunga sambamba na kupata burudani yao ya soka, kwani washambuliaji hao wanalijua boli.
“Wote hao ni pendekezo la kocha Benchikha, tunaamini ujio wa washambuliaji utaongeza kitu katika timu, kutokana na ubora wao waliotoka nao katika timu zao wakiwa wanacheza katika vikosi vya kwanza,” amesema Ahmed.